Wananchi watapata huduma salama za dijitali, asema Waziri Ndung’u

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa dijitali Dkt. Margaret Ndung’u.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa dijitali Dkt. Margaret Ndung’u ametoa wito kwa maafisa wakuu wa sekta ya ICT kutumia fursa ya misingi imara ya uwekezaji katika sekta hiyo.

Kwenye hotuba yake wakati wa sherehe ya kufungwa kwa mpango wa kuwapa mafunzo makatibu na wakurugenzi katika idara ya teknolojia ya habari na mawasiliano iliyoandaliwa katika chuo cha mafunzo ya uongozi cha Lower Kabete, Waziri huyo alisema kuwa ni sharti upatikanaji wa huduma za dijitali uwe jumuishi, wazi na salama kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wote.

“Kama watumishi wa umma katika karne ya 21, mna fursa ya kubadili siku za usoni na kuchangia mabadiliko katika sekta ya ICT,” alisema Dkt. Ndung’u.

Vile vile, alikariri haja ya kutumia teknolojia ibuka kuimarisha ubunifu na vitengo vipya vikiwemo uhandisi wa programu, utekelezaji biashara mtandaoni na utengenezaji bidhaa ili kuboresha uchumi wa dijitali.

Dkt. Ndung’u pia alisema kuwa ipo haja ya kukabiliana na hatari zilizoko kwa kuimarisha usalama wa mtandaoni na mbinu za ushughulikiaji takwimu humu nchini kuambatana na kanuni za kimataifa.

Share This Article