Wananchi waonywa dhidi ya kuanguka kwa kifaa kutoka angani

Tom Mathinji
2 Min Read
Shirika la Anga la Kenya.

Shirika la Anga la Kenya (KSA), limeonya kuna uwezekano wa vipande vya mabaki ya chombo cha anga za juu kwa jina Norad, kuanguka hapa nchini kati Jumamosi na Jumapili.

KSA imesema kuwa kifaa hicho kinatarajiwa kuanguka Jumamosi tarehe 19 Aprili 2025, saa tano na dakika kumi na tano usiku, lakini pia kuna uwezekano wa kuchelewa au kutangulia kwa muda wa hadi saa 15 na dakika 46.

Kupita kwa taarifa, shirika hilo limedokeza kuwa chombo hicho kitapitia anga ya Mashariki mwa Afrika, ikiwa ni pamoja na Kenya, kuelekea Tanzania na kwingineko.

“Shirika la Anga la Kenya, linafahamisha umma kuhusu kuanguka kwa kifaa kutoka angani Norad ID 61909/2024-205R, ambacho ni sehemu ya vifusi kutoka kwa roketi,” ilisema KSA kwenye taarifa.

Licha ya kwamba KSA, haijasema wazi kifaa hicho kitaanguka upande upi wa nchi, wananchi wameshauriwa kutoa taarifa kwa maafisa wa polisi au afisi yoyote ya serikali, watakapoona kifaa chochote kikubwa kutoka angani katika maeneo yao.

“Shirika la Anga la Kenya, linashirikiana na washirika wengine kubaini mahali kifaa hicho kitaanguka na wakati upi,” iliongeza taarifa ya KSA.

Shirika hilo limesema kuwa kifaa hicho ni hatari kwa maisha na mali ya watu, kutokana na ukubwa wake.

Mnamo mwezi  Januari 2025, kifaa cha chuma kilichoaminika kuwa mabaki ya roketi kilianguka katika kijiji cha Makuku, kaunti ya Makueni, na kusababisha wasiwasi miongoni mwa wakazi.

TAGGED:
Share This Article