Gavana wa kaunti ya kwale Fatuma Achani amewataka wanakandarasi wa barabara katika kaunti ya Kwale kuharakisha kukarabati barabara zilizoharibiwa wakati wa msimu wa mvua ya Elnino.
Mvua hiyo ilisababisha kuharibika kwa barabara nyingi za kaunti ya Kwale na kutatiza shughuli za usafiri.
Achani alikuwa ameandamana na Naibu wake Chirema Kombo katika uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya lami kwa awamu ya pili ya mkilo-kalalani na Mavirivirini huko Mwavumbo eneo la kinango kwa gharama ya shilingi milioni 260.
Alisema kuwa uboreshaji wa miundo msingi ya barabara unaotekelezwa na serikali yake unalenga kuimarisha sekta ya uchukuzi na biashara katika kaunti hiyo hasa kwa wakulima wanaopaswa kupeleka mazao yao sokoni bila usumbufu wa barabara mbovu.
Mapema wiki hii Gavana Achani pia Alizindua ujenzi wa barabara nyingine ya lami ya tiwi sokoni hadi vinuni inayounganisha wakazi wa eneo hilo la Matuga na barabara kuu ya kombani -Kwale kwa gharama ya shilingi milioni 226
Ujenzi wa barabara hizo za lami unaambatanishwa na kuwekwa kwa taa za usalama zinazotumia miale ya jua katika barabara husika.