Rais wa Marekani Joe Biden anatoa msamaha kwa wanajeshi wa zamani wa nchi yake waliokamatwa, kushtakiwa na kuhukumiwa chini ya sheria ya zamani iliyoondolewa ambayo ilipiga marufuku mahusiano ya watu wa jinsia moja nchini humo.
Katika taarifa Rais Biden ametangaza kwamba msamaha wake umechochewa na haja ya kurekebisha kosa la kihistoria na sasa wanajeshi hao wa zamani wataondolewa mashtaka dhidi yao.
Biden alilalamika kwamba hata ingawa watu hao walijitolea kuhudumia nchi yao, walistaafishwa kutoka kwenye jeshi kutokana na mapendeleo yao ya kimapenzi.
“Wengine kati ya wanajeshi hawa wa zamani walishtakiwa kwenye mahakama za kijeshi na wamebeba mzigo wa hujuma hii kwa miaka mingi.” ilisema taarifa ya Biden.
Watakaonufaika na msamaha wa Rais Biden ni wale walioshtakiwa kwa ulawiti chini ya kifungu nambari 125 cha sheria ya haki katika jeshi. Sheria hiyo ilianza kutumika mwaka 1951 na ikafanyiwa marekebisho mwaka 2013 ili kutumika kwa visa vya kulazimishwa pekee.
Walihukumiwa kabla ya kuanzishwa kwa sera ya kutouliza na kutosema kuhusu mapendeleo ya kingono mwaka 1993 ambayo ilisaidia kuwakinga wanajeshi waliokuwa kwenye mahusiano jinsia moja.
Mwaka 2011 bunge la Marekani liliruhusu watu hao kuhudumu wazi wazi katika jeshi.
Sasa wanaweza kutuma maombi ya kupata ithibati ya kudhihirisha kwamba wameondoewa lawama na sababu za kuondolewa katika jeshi zibadilishwe ili waweze kudai malipo yao.
Msamaha wa Rais Biden unajiri wakati watu wa mahusiano ya jinsia moja na wengine almaarufu LGBTQ wanaadhimisha mwezi wao unaofahamika kama “Pride Month”.