Jeshi la Sudan na makundi ya wapiganaji yanayowasaidia wameingia katika eneo la Wad Madani na wanafukuza wapiganaji wa kundi la RSF, kutoka jiji hilo muhimu la jimbo la Gezira.
Haya ni kulingana na jeshi.
Katika taarifa Jumamosi, Jeshi lilipongeza watu wa Sudan kufuatia hatua ya wanajeshi ya kuingia katika jiji la Wad Madani mapema Jumamosi, baada ya eneo hilo kuwa chini ya udhibiti wa RSF kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba sasa wanajeshi hao wanajitahidi kurejesha maeneo ambayo bado yanadhibitiwa na RSF jijini humo.
Kundi la RSF halikusema lolote kuhusu tukio hilo.
Afisi ya msemaji wa jeshi na wapiganaji na waziri wa mawasiliano na utamaduni Khalid al-Aiser ilisema jeshi limekomboa jiji hilo huku jeshi likichapisha video inayoonyesha wanajeshi ndani ya Wad Madani.
Jeshi la Sudan na kundi la RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023, na kusababisha kile kilichotajwa na umoja wa Mataifa kuwa tatizo baya zaidi ulimwenguni la watu kupoteza makazi na kukumbwa na baa la njaa.
Jiji la Wad Madani ni muhimu kwa sababu ni makutano ya njia kadhaa kuu zinazounganisha majimbo mengi na ndio mji mkuu ulio karibu na jiji kuu Khartoum.
Pande zote mbili, jeshi la Sudan na kundi la RSF zimelaumiwa kwa kutekeleza uhalifu unaojumuisha kulenga raia na kushambulia maeneo ya makazi kiholela.