Wanajeshi wa Israel wamechoma na kubomoa makazi kadhaa katika eneo la Rafah ambalo liko kusini mwa ukanda wa Gaza. Haya yanafuatia shambulizi lililotekelezwa na wapiganaji wa Hamas.
Wanajeshi wanane wa Israel wanasemekana kuuawa katika shambulizi hilo ambalo waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelitaja kuwa gharama nyingine kubwa kwa jeshi la Israel linalopigana vita vya haki huko Gaza.
Katika upande wa kaskazini mwa ukanda wa Gaza, wapalestina wapatao 28 wameripotiwa kufariki katika mashambulizi ya bomu ya Israel katika makazi matatu.
Wakati huo huo shirika la kushughulikia wakimbizi wapalestina la umoja wa mataifa UNRWA limeonya kwamba watoto wapatao elfu 50 wanahitaji matibabu ya haraka ya utapiamlo katika ukanda wa Gaza.
Kufikia sasa watu elfu 37,296 wameuawa na wengine elfu 85,197 kuachwa na majeraha katika vita vya Israel katika ukanda wa Gaza tangu vilipoanza Oktoba 7, 2023.