Wanajeshi nchini Niger wanadai kwamba walimng’oa mamlakani Rais Mohamed Bazoum jana Jumatano, Julai 26, 2023, saa chache baada ya walinzi wake kumzuilia katika ikulu.
Katika tangazo kwenye runinga ya kitaifa ya Niger, Kanali Mkuu Amadou Abdramane alisema wanajeshi na vikosi vingine vya usalama waliamua kusitisha utawala ambao wananchi walikuwa wameuzoea.
Abdramane alisema hatua yao ilichochewa na kuzorota kwa usalama na usimamizi mbaya wa masuala ya kijamii na kiuchumi.
Wanajeshi hao wamefunga mipaka ya nchi ya Niger na kuweka amri ya kutotoka nje kote nchini humo. Taasisi zote pia zimesimamishwa.
Wakati wa kutoa tangazo hilo, Abdramane alionekana ameketi akiwa amezingirwa na maafisa wengine ambao walikuwa wamevaa sare rasmi za kazi. Kundi hilo ambalo linajiita “Baraza la Kulinda Nchi” limeonye dhidi ya hatua yoyote ya kujaribu kuingilia kati kutoka mataifa mengine.
Tangazo hilo linajiri baada ya siku ya sintofahamu baada ya afisi ya Rais nchini Niger kutangaza kuwa Ikulu ya Rais ilikuwa imezingirwa na maafisa wa kundi la kumlinda kiongozi wa nchi.
Haijulikani Rais Bazoum alikuwa wapi wakati wa tangazo la Abdramane wala haijulikani kama amejiuzulu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitangaza kwamba alizungumza na Rais wa Niger kwa njia ya simu na akamhakikishia kwamba Marekani inamuunga mkono na inatambua kwamba yeye ndiye alichaguliwa kuongoza nchi hiyo kidemokrasia.
Hili ni jaribio la saba la kupindua serikali katika eneo la magharibi na kati mwa Afrika tangu mwaka 2020 na huenda yanayojiri yakatatiza juhudi za nchi za magharibi kusaidia nchi za eneo la Sahel kukabiliana na makundi ya waasi kama al-Qaeda na ISIS.