Wanafunzi wa zamani wa shule ya msingi ya Nyandarua wamezindua kampeni ya ujenzi wa maktaba ya kisasa ya gharama ya shilingi milioni 70 shuleni humo kama njia ya kuibadili mfumo wa masomo shuleni humo.
Mpango huo unaolenga kuboresha elimu mashinani utahakikisha wanafunzi wa kaunti za Nyandarua na Laikipia wanapata vifaa vya masomo vya ubora wa hali ya juu na fursa nyinginezo.
Itakapokamilika, maktaba hiyo itahudumia wanafunzi wapatao elfu moja wanaosomea katika taasisi hiyo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Charles Mbugua alielezea kuridhika kwake na mpango huo huku akisimulia jinsi ameshuhudia kukua kwa chama cha wanafunzi wa zamani wa shule hiyo kwa miaka 13 sasa.
Matamshi yake yalikaririwa na Magdalene Wanjugu ambaye anaongoza utekelezaji wa mradi huo. Wanjugu alisema maktaba hiyo ya kidijitali inatumia teknolojia ya kisasa ambayo itawezesha wanafunzi kushindana na wenzao ulimwenguni.
Wanafunzi nao walionyesha furaha yao na mradi huo ambao wanaamini utabadili jinsi wanasoma na wataweza kupata vitabu na mitihani ya awali ili kujitayarisha vilivyo.