Wanafunzi wa chekechea Machakos kufurahia maziwa ya bure

Martin Mwanje
1 Min Read

Gavana wa kauti ya Machakos Wavinya Ndeti jana Alhamisi alizindua mpango wa maziwa ya bure kwa wanafunzi wote wa chekechea, ECDE katika shule za umma katika kaunti hiyo.


Mpango huo ulizinduliwa katika shule ya msingi ya Kyemutheke katika kaunti ndogo ya Mavoko.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliopewa jina “Maziwa ya Mama,” Gavana Ndeti aliusifia mpango huo akiutaja kuwa hatua kubwa itakayoongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule, itakayoboresha lishe miongoni mwa watoto na pia kuboresha afya yao.


Kando na mafao hayo, mpango huo unatarajia kupiga jeki mapato ya wakulima wa maziwa katika kaunti hiyo.

“Fursa hii kwa wakulima wetu ni hatua kuelekea kufikiwa kwa ajenda yangu ya maendeleo ya ‘Chakula Mezani, Pesa Mfukoni,'” aliongeza Gavana Ndeti.

Share This Article