Wanachama wa ODM wateuliwa kuwa Mawaziri

Martin Mwanje
2 Min Read

Wanachama kadhaa wa ODM, wengine ambao wanahudumu kwa sasa kama wabunge, wameteuliwa na Rais William Ruto kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri. 

Wao ni pamoja na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Opiyo Wandayi. Wandayi ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati akichukua mahali pa Davis Chirchir aliyehamishiwa Wizara ya Barabara na Uchukuzi.

Mbunge mteule John Mbadi ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Fedha, wadhifa ambao awali ulishkiliwa na Prof. Njuguna Ndung’u.

Magavana wawili wa zamani ambao ni wanachama wa ODM pia nao wameteuliwa kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri.

Wao ni aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika huku aliyekuwa Gavana wa Mombasa akiteuliwa kuwa Waziri wa Madini. Simon Chelugui ndiye aliyekuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika katika Baraza lililovunjwa la Mawaziri huku Salim Mvurya akiwa Waziri wa Madini. Mvurya sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara huku Chelugui akipoteza wadhifa wake.

Kumekuwa na hali ya kuvuta ni kuvute katika chama cha ODM juu ya ikiwa wanachama wa chama hicho wanastahili kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri au la.

Jana Jumanne, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema chama hicho hakina mipango ya kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza, msimamo ambao ulipingwa vikali na mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma.

Ingawa Gavana wa Siaya James Orengo pia alipinga wanachama wa ODM kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza, mbunge mteule John Mbadi ambaye sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha alipinga msimamo huo akisema kuna haja kwa wanachama wa ODM kujiunga na serikali kwa manufaa ya taifa.

Isipokuwa ODM, vyama tanzu vya Azimio vikiongozwa na Kalonzo Musyoka wa Wiper vilipinga vikali wanachama wa muungano huo kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza.

Inasubiriwa kuona hatima ya muungano huo ikizingatiwa kwamba kiongozi wake Raila Odinga ameridhia wanachama wake kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri.

Share This Article