Hatima ya waziri wa kilimo Mithika Linturi sasa imo mikononi mwa kamati ya muda ya bunge la taifa inayojumuisha wanachama 11.
Hii ni baada ya wabunge kuidhinisha hoja ya kutaka kubanduliwa kwa waziri huyo na kutoa nafasi ya kubuniwa kwa kamati maalum itakayochunguza madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka dhidi ya waziri huyo hasa katika sakata ya mbolea ghushi.
Hoja hiyo ilitimiza vigezo vya kuungwa mkono na angalu wabunge 117 hasa baada ya kuungwa mkono na wabunge 149.
Wabunge 36 walipinga hoja hiyo huku watatu wakikosa kupiga kura. Awali hoja hiyo ya kutaka kumbandua afisini waziri huyo iliyowasilishwa na mbunge wa Bumula Nelson Wamboka ilizua mjadala mkali bungeni.
Mjadala ulikumbwa na sarakasi nyingi huku wabunge wakikuka tararibu wakati mmoja na kupiga kelele.
Kamati hiyo inayojumuisha wabunge sita wa chama cha UDA, wanne wa muungano wa Azimio na mmoja kutoka chama cha Jubilee inatarajiwa kuwasilisha mapendekezo yake baada ya muda wa siku kumi.
Wanachama hao kumi na moja ni pamoja na Naomi Waqo, Robert Mbui, Rachael Nyamai, Samuel Kiprono Chepkonga, George Murungara, T. J. Kajwang, Moses Malulu Injendi, Jane Njeri Maina, Kassim Sawa Tandaza, Catherine Omanyo na Yusuf M. Farah.
Iwapo kamati hiyo itampata Linturi na hatia, bunge litapiga kura ya kumwondoa afisini. Hata hivyo iwapo haitampata na hatia, hoja hiyo itatupiliwa mbali.