Wanablogu wataka haki itendeke kuhusu mauaji ya mwenzao

Marion Bosire
2 Min Read

Wanablogu humu nchini wanataka hali itendeke kwenye kisa cha mauaji ya kutatanisha ya mwenzao wa kaunti ya Meru Daniel Muthiani, maarufu kama Sniper.

Mwakilishi wa wadi ya Kileleshwa katika kaunti ya Nairobi Robert Alai ambaye pia ni mwanablogu alitoa taarifa Jumapili Disemba 17, 2023 jioni kwa niaba ya wanablogu nchini akitaka haki itendeke kwa mauaji ya Sniper.

Katika taarifa hiyo, Alai alizitaka afisi za upelelezi wa jinai na ile ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ziharakishe uchunguzi kuhusu mauaji hayo na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Kiongozi huyo alitoa wito kwa washikilizi wa nyadhifa za umma kukubali ukosoaji, uchunguzi na maswali magumu, vitu ambavyo kulingana naye ni muhimu katika nchi yoyote huru inayoongozwa na katiba.

Huku akikiri kwamba kazi ya uanablogu sio rahisi, Alai aliorodhesha baadhi ya wanablogu nchini na magumu ambayo wamepitia.

Kwa upande wake, katibu wa masuala ya kidijitali wa Rais William Ruto Dennis Itumbi, aliomba watumishi wa umma kutoumiza wanablogu kwa njia yoyote ile kwa kutoa maoni yao kuhusu utendakazi wao.

Daniel ambaye ni mwenyeji wa Igembe ya kati na ambaye alikuwa akikosoa uongozi wa kaunti ya Meru kwenye mitandao ya kijamii anasemekana kutoweka baada ya kudaiwa kwenda kukutana na mtu asiyefahamika aliyeahidi kufanya kazi naye ili kuendeleza maslahi ya kisiasa kwa wakazi wa Meru.

Waziri wa usalama Kithure Kindiki awali alikuwa ametoa wito kwa afisi ya upelelezi wa jinai kuharakisha uchunguzi kuhusu kutoweka kwa mwanaharakati huyo ambaye sasa amebainika kuuawa.

Share This Article