Wanabiashara Meru wasema siasa inaathiri biashara

Marion Bosire
1 Min Read

Wafanyabiashara katika kaunti ya Meru wanalalamika kwamba siasa mbaya inayoendelea katika eneo hilo inaathiri biashara.

Akizungumza na wanahabari wa shirika la KBC katika afi yake mjini Meru, mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara katika kaunti ya Meru Joshua Mungania alisema kwamba siasa hiyo imesababisha wawekezaji waogope kuwekeza katika kaunti hiyo.

Wafadhili nao alisema wameanza kujiondoa kwenye miradi mbali mbali.

Mungania kwa niaba ya wafanyabiashara, aliomba wanasiasa wa kaunti ya Meru wapunguze joto la siasa wafanye mazungumzo ili kutuliza hali.

Alisema wafanyabiashara wako tayari kupatanisha viongozi wanaozozana katika kaunti hiyo ya Meru suluhisho la kudumu lipatikane ili kaunti hiyo iweze kusonga mbele.

Mwenyekiti huyo wa chama cha wafanyabiashara kaunti ya Meru, aliwataka viongozi waliochaguliwa kutafuta huduma za watu mashuhuri katika jamii ya Meru ili wawapatanishe.

Alisema iwapo hilo litafanyika, amani na maendeleo vitapatikana na kwamba sasa mwananchi wa kawaida anaathirika kwa kutopata huduma na maendeleo kutoka kwa uongozi wa kaunti.

Share This Article