Mbunge wa Bumula Jack Wamboka ameitaka serikali kuufanyia mabadiliko mfumo mpya wa kufadhili elimu vyuoni akiutaja kuwa ghali kwa Wakenya.
Wamboka ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu usimamizi na uwekezaji wa umma ,amesisitiza kuwa serikali yapaswa kugharimia mfumo wa elimu ya umilisi – CBC ili kuwapunguzia wazazi mzigo wa masomo.
“Wazazi maskini wameshindwa kugharimikia elimu ya watoto wao kwa sababu mfumo wa sasa unagharimu pesa nyingi,”alilalama Wamboka.
Akizungumza katika eneo bunge la Tongaren, mbunge huyo alisema ufadhili wa sasa wa elimu unawapendelea wanafunzi wa matajiri.
Ameitaka serikali kutoharakisha utekelezaji kikamilifu mfumo wa CBC ambao ulikuwa mzuri ila watekelezaji sera wameshindwa kujukumika ipasavyo.
Wamboka amesisitiza haja ya serikali kukabili changamoto zinazokabili mfumo huo zikiwemo upungufu wa walimu wa kutosha, ukosefu wa vifaa vya masomo, ukosefu wa hela na ufisadi uliokithiri.