Gavana wa Siaya James Orengo ameagiza kutolewa kwa shilingi Milioni 9.8 zinazodaiwa na wauguzi wa kaunti hiyo, kwa muda wa miaka mitatu sasa.
Orengo alisema ni makosa kushikilia mishahara hiyo ya miezi miwili ya wauguzi hao, wakati wa kipindi walichoshiriki mgomo mwaka 2021.
Gavana huyo alisema kuwa mkataba wa kurejea kazini ulitiwa saini, akidokeza kuwa wauguzi hao walishinda kesi katika mahakama ya kushughulikia maswala ya wafanyakazi na hivyo serikali ya kaunti hiyo haina budi kuwalipa mishahara yao.
Orengo aliyasema hayo katika makao makuu ya kaunti ya Siaya, alipokuwa akiwahutubia wauguzi hao walioandamana hadi afisni mwaka kuitisha malipo hayo.
Alisema kaunti hiyo haina sababu yoyote ya kuendelea kushikilia fedha hizo.