Serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote aliyetepetea na kusababisha ajali mbaya ya barabarani iliyotokea huko Nyeri ambapo watu wapatao 16 waliangamia na wengine wengi kuachwa na majeraha.
Katika taarifa, Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir alisema wizara hiyo itashirikiana kwa karibu na Halmashauri ya Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA kuchunguza ajali hiyo ya juzi Jumamosi jioni.
Chirchir alisema watakaopatikana na hatia ya kutepetea na kusababisha ajali hiyo watachukuliwa hatua kali akihimiza waendeshaji magari kuwa makini, kuzingatia sheria na kujali wengine wanaotumia barabara.
Huku hayo yakijiri, jamaa za walioangamia walikusanyika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya kaunti ya Nyeri kwa ajili ya kutambua miili ya wapendwa wao wakiwa wamejawa huzuni.
Kamanda wa Trafiki katika eneo la katikati mwa nchi Elizabeth Vivi alisema kwamba miili 10 ilitambuliwa jana huku mingine ikiwa bado haijatambuliwa.
Ajali hiyo ilitokea Jumamosi jioni katika eneo la Yunis, kwenye barabara ya kutoka Nyeri kuelekea Mweiga na ilihusisha gari la kubeba abiria na lori.
Rais William Ruto alitoa pole zake huku akiahidi usaidizi wa serikali kuu kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Nyeri kwa waathirwa.