Waliomwibia mhubiri wakamatwa

Marion Bosire
2 Min Read

Watu watatu wanaoshukiwa kumteka nyara na kumwibia mhubiri mmoja simu ya mkononi na pesa Alhamisi usiku alipokuwa akiingia kwenye mkahawa mmoja karibu na uwanja wa michezo wa Nyayo wamekamatwa.

Bernard Mbunga Mbusu, Alphonce Munyau na Samuel Musembi Kamito walikamatwa katika makazi yao kwenye maeneo ya Syokimau, Kitengela na Kamito mtawalia katika oparesheni iliyoongozwa na maafisa wa upelelezi wa jinai wa kaunti Nairobi.

Mwathiriwa ambaye ni mhubiri katika kanisa la Christ Church, alielezea kwamba alikuwa anakwenda kupata chajio baada ya shughuli nyingi za maandalizi ya mkutano wa injili wa Benny Hinn katika uwanja wa Nyayo wakati wanaume hao walimkamata na kumwingiza kwenye gari.

Katika gari hilo, mhubiri huyo alivuliwa nguo, akapigwa picha na kisha kulazimishwa kuwapa nambari ya siri ya Mpesa au picha hizo zisambazwe mitandaoni. Washukiwa hao walijitumia shilingi elfu 55 kabla ya kumwachilia.

Mhubiri huyo alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha uwanja wa michezo wa Nyayo ambapo maafisa wa DCI walianzisha uchunguzi mara moja uliowaelekeza katika jumba la makazi la Village Apartmentmlango nambari F2 huko Syokimau ambapo mshukiwa wa kwanza Bernard Mbunga Mbusu alikamatwa.

Simu tatu za rununu moja ikiwa iliyotumiwa pesa za mhubiri huyo zilipatikana kwenye nyumba ya Benard.

Bernard baadaye alielekeza maafisa wa uchunguzi hadi walikokuwa wenzake wawili na wote sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Langata wakisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Share This Article