Raia wawili wa Uganda wamekamatwa kwa kosa la kumtukana Rais Yoweri Museveni, mkewe Janet Museveni na mwanao Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kwenye TikTok.
Jaji Stella Maris Amabilis aliamuru kuwa David Ssengozi, mwanzilishi wa Lucky Choice wa umri wa miaka 21 na Isaya Ssekagiri wa umri wa miaka 28, warudishwe rumande katika gereza la Kigo hadi leo Jumatano, wakitarajiwa kufikishwa mahakamani.
Wanadaiwa kutumia matamshi ya chuki na kueneza habari mbaya kuhusu familia ya rais na wanamuziki wanaohusishwa na chama tawala cha Uganda.
Walipofika mahakamani Jumatatu, wawili hao walikanusha mashtaka dhidi yao.
Wanashtakiwa pamoja na Julius Tayebwa wa miaka 19, ambaye tayari amefikishwa mahakamani na bado yuko gerezani kwa makosa sawa na hayo.
Waendesha mashtaka wanasema waliochapisha habari hizo kwenye TikTok wanalenga ‘kukashifu, kudharaulisha na kueneza chuki’ dhidi ya familia ya Rais Museveni na watu wengine.
Hakimu aliidhinisha kuzuiliwa kwao baada ya polisi kusema kuwa bado wanachunguzwa.
Septemba 9 mwaka huu, msemaji wa jeshi la polisi nchini Uganda, Rusoke Kituuma alionya kuwa kumtukana rais ni kosa.
Haijabainika ni ujumbe gani uliosababisha kukamatwa kwake, lakini katika video iliyochapishwa kwenye TikTok tarehe 4 Aprili mwaka huu kwenye ukurasa wa LuckyChoice70, wenye kichwa ‘maadui wangu wa kwanza’ aliikosoa familia ya rais kwa kutumia lugha chafu zinazohusiana na ngono.