Udanganyifu wa mitihani: KUPPET yatishia kwenda mahakamani

Marion Bosire & Jeff Mwangi
2 Min Read

Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vuo, KUPPET kimetishia kuelekea mahakamani iwapo walimu wakuu wa shule za sekondari wataadhibiwa na Tume ya Kuajiri Walimu, TSC kwa sababu ya udanganyifu wa mtihani.

Akizungumza wakati wa mkutano wa mkuu wa tawi la Meru la chama cha KUPPET, Katibu Mkuu wa chama hicho Akello Misori alisema inasikitisha kwamba serikali imeanzisha adhabu kali dhidi ya walimu wakuu wa shule udanganyifu unaporipotiwa katika shule zao.

Misori anashikilia kwamba kuvujishwa kwa mitihani huanzia kwenye baraza la mitihani ya kitaifa, KNEC kabla ya kufika kwenye makasha ya kuhifadhi yanapochukuliwa na wasimamizi wa vituo.

Aliongeza kuwa wameafikia hatua hiyo ili maafisa wote waliohusika na usimamizi wa mitihani wakiwemo wale wa KNEC, TSC na hata Waziri wa Elimu wafike mahakamani kuelezea jinsi mwalimu mkuu wa shule anaweza kuhusika katika udanganyifu wa mtihani kabla ya hatua kuchukuliwa dhidi yake.

Chama hicho kitakwenda mahakamani pia kutafuta maagizo ya kukomesha hatua ya kuhamishahamisha walimu wanaosimamia mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, KCSE wakisema inavuruga shughuli nzima na hata kusababisha matumizi zaidi ya fedha katika usafiri wa walimu hao.

Kuhusu sekondari ya chini, JS, Misori alipendekeza serikali kubadili msimamo na kuacha shule hizo ziwe katika shule za sekondari kwani kwa sasa usimamizi sio mzuri zikiwa katika shule za msingi.

Marion Bosire & Jeff Mwangi
+ posts
Share This Article