Walimu wataka taasisi za elimu ziboreshwe Lamu

Marion Bosire
1 Min Read

Walimu katika shule za Jipendeni na Lumshi ambazo ziko katika wadi ya Witu, eneo bunge la Lamu Magharibi kaunti ya Lamu, wamepaaza zauti zao kuangazia hali duni ya taasisi za elimu katika maeneo hayo.

Matatizo wanayokumbana nayo ni pamoja na ukosefu wa walimu waliohitimu na miundomsingi duni katika shule nyingi za maeneo hayo.

Kulingana na walimu hao, wanafunzi ni wengi kupita kiasi katika kila darasa hali ambayo inafanya iwe vigumu kwao kuangazia kila mwanafunzi binafsi.

Wazazi na watu wengine wa jamii ya eneo hilo wanatatizwa na athari za hali hiyo kwa maendeleo ya wanafunzi kimasomo.

Paa za madarasa mengi zinavuja huku kuta zikianguka na kuhatarisha maisha ya wanafunzi na ya walimu.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Jipendeni anaelezea kwamba shule yake ina walimu watano walioajiriwa na TSC huku wengine watano wakiwa wa muda.

Hali hiyo kulingana naye inatosheleza wanafunzi 450 pekee na sio idadi ya sasa ya wanafunzi zaidi ya 600.

Mvua kubwa iliyoshuhudiwa hivi maajuzi ilifanya hali kuwa mbaya zaidi ambapo vyoo vingi viliporomoka na kulazimisha wanafunzi wa kike na wa kiume kutumia vilivyosalia.

Walimu, wazazi na wadau wa elimu katika eneo hilo sasa wanaomba serikali kuu na serikali ya kaunti kuchukua hatua.

Share This Article