Walimu wakuu waonywa dhidi ya kuomba wazazi fedha zaidi

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amewaonya walimu wakuu wa shule zote za umma nchini dhidi ya kuitisha fedha zaidi kutoka kwa wazazi.

Amesema shilingi bilioni 62 za kugharimia masomo tayari zimesambazwa kwa shule zote.

Shilingi zingine bilioni 10 zimetolewa kwa hazina ya kitaifa ya maendeleo ya maeneo bunge, NG-CDF ili ufadhili wa masomo utolewe kwa wanaouhitaji.

Kulingana na Rais Ruto, walimu wengine elfu 20 wataajiriwa ili kuhakikisha elimu ya ubora wa hali ya juu kwa wanafunzi wote.

Akizungumza wakati wa ibada katika shule ya msingi, Rais Ruto aliahidi kujitolea kwa serikali yake kumaliza kero la njaa nchini.

Ili kufanikisha hilo, alisema ekari elfu 10 za ardhi zitawekwa chini ya mpango wa unyunyiziaji mashamba maji ili kuimarisha uzalishaji wa mpunga.

Bilioni 1.7 zimetengwa ili kulipa madeni ya wakulima wa miwa mwezi ujao katika lengo la kufufua sekta ya sukari.

Rais Ruto amewataka Wakenya wote kukumbatia kilimo ili kupunguza kiwango cha chakula kinachoagizwa kutoka nje na kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula.

Share This Article