Walimu wa JSS wafanya maandamano Ol-Kalou

Marion Bosire
1 Min Read

Walimu wa shule za sekondari msingi katika kaunti ya Nyandarua walifanya maandamano mjini Ol-Kalou kulalamikia walichokitaja kuwa kuhadaiwa na serikali katika masuala ya ajira na mishahara.

Walimu hao waliokuwa wamejawa ghadhabu walilalamika kwamba waahidiwa ajira ya kudumu na malipo ya uzeeni baada ya mwaka mmoja wa kuhudumu kama wanagenzi lakini hilo halikufanyika.

Sasa wanasema kwamba wanalazimishwa kutia saini mikataba mingine ya kuhudumu kama wanagenzi hata baada ya mahakama kufafanua kwamba mikabata ya uanagenzi ni kinyume cha sheria.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama chao Peter Maina, walimu hao walilalama kwamba malipo ya shilingi elfu 17 kila mwezi ni kidogo sana na hayatoshelezi mahitaji yao yote na wanataka wafidiwe kwa miwezi 12 ambayo wamehudumu.

Pesa wanazotaka kama fidia ni shilingi 480,000 pamoja na ajira ya kudumu na malipo ya uzeeni.

Jambo lingine walilolalamikia ni ubaguzi katika uajiri baada ya jukumu la kuajiri kukabidhiwa wabunge wakisema ufisadi umekithiri katika shughuli nzima ambapo waliofuzu zaidi ya miaka mitano iliyopita wanakosa fursa za ajira huku waliofuzu hata mwaka jana wakipata.

Wametishia kugoma na kulemaza shughuli za masomo shule zitakapofunguliwa iwapo serikali haitachukua hatua kushughulikia malalamishi yao.

Share This Article