Serikali ya kaunti ya Kericho itawaajiri walimu wa kudumu 1,115 wa shule ya chekechea, ECDE mwezi Agosti mwaka huu.
Walimu walio na vyeti katika ECDE watapokea mshahara wa shilingi 25,000; wa stashahada shilingi 35,000, ilhali wale walio na shahada watapokea mshahara wa shilingi 44,000.
Akizungumza katika eneo la Moronget, wadi ya Kipkelion wakati wa uzinduzi wa darasa la ECDE na vitabu vya kiada vyenye thamani ya shilingi milioni 7, Gavana Eric Mutai alisema serikali yake imejitolea kumaliza mateso wanayokumbana nayo walimu kwa sababu ya kulipwa mishahara duni.
Mutai alisema mpango wa lishe ya wanafunzi wa ECDE pia utaanzishwa kuanzia mwezi Agosti.