Walanguzi wawili wanaswa na bangi ya thamani ya shilingi milioni tisa Isebania

Tom Mathinji
1 Min Read
Bangi ya thamani ya shilingi milioni tisa yanaswa Isebania.

Polisi katika kituo cha Isebania kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania kaunti ya Migori, wamenasa bangi ya thamani ya shilingi milioni tisa iliyokuwa ikisafirishwa kuingizwa nchini Kenya.

Kulingana na kamanda wa polisi kaunti ya Migori Francis Nguli, bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwa gari aina ya Prado SUV lenye nambari ya usajili KCL 532E, kabla ya kunaswa na maafisa wa polisi.

Washukiwa wawili waliotambuliwa kuwa Daniel Okoth na Erick Ombima walikamatwa tayari wakiwa nchini wakipitia barabara ya Nyametaburo na kuunganisha na barabara ya Isebania-Migori kwenye eneo la Mabera, Migori.

Takriban kilo 300 ya bangi ilipatikana ndani ya gari. Lilipofika katika daraja la Karamu, polisi waliwatokea kwa ghafla.

Dereva wa gari hilo, alijaribu kumkanyaga polisi mmoja katika juhudi za kukwepa kizuizi cha barabara lakini gurudumu la gari hilo lilipasuliwa kwa risasi na dereva kulazimishwa kusimama.

Washukiwa watatu walikuwa kwenye gari hilo lakini mmoja wao alifanikiwa kutoroka kwa miguu.

Wawili hao walifikishwa mahakama ya Kehancha na kushtakiwa kwa kosa la kumiliki dawa za kulevya.

TAGGED:
Share This Article