Maafisa wa polisi nchini Bolivia wamekamata wakuu wawili wa jeshi baada ya hatua ya kutuma wanajeshi na zana za kivita kwenye afisi za serikali, hatua ambayo Rais Luis Arce aliitaja kuwa jaribio la mapinduzi.
Waliokamatwa ni mkuu wa jeshi kwa jumla Juan Jose Zuniga na mkuu wa jeshi la wanamaji Juan Arnez Salvador.
Wanajeshi waliingia katika jengo la Plaza Murillo, jijini La Paz huku kifaru cha jeshi kikijaribu kuingia katika makazi rasmi ya rais katika jiji hilo hilo.
Akiwa amezungukwa na wanajeshi na zana zao za kivita kabla ya kukamatwa, Zuniga calisema kwamba lengo lao ni kurejesha mfumo mwafaka wa demokrasia nchini humo.
Baada ya muda Zuniga alikamatwa na maafisa wa polisi akihutubia wanahabari huku Rais Arce akipaaza sauti kutoka kwenye roshani ya makazi yake akisema hakuna mtu ambaye angeweza kuchukua demokrasia ambayo wamejishindia.
Rais huyo alikuwa amehimiza wananchi wa Bolivia kupigania na kulinda demokrasia yao kwenye ujumbe aliotoa awali kupitia runinga ambapo alikuwa amezungukwa na mawaziri wa serikali yake katika ikulu.
Lakini katika hatua nyingine ya kukanganya, Zuniga ambaye alifutwa kazi mara moja aliambia wanahabari kabla ya kukamatwa kwamba aliagizwa na Rais kufanya alivyofanya ili kuchochea oparesheni itakayomwonyesha kuwa na mamlaka zaidi.
Zuniga alielezea kwamba hayo yalifanyika katika mkutano wa Jumapili.