Wakulima zaidi ya 100 kutoka kaunti ya Kericho wameishutumu serikali na Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) kwa kuchelewa kuwapa mbolea.
Wakulima hao walitembelea ghala ya NCPB katika kaunti hiyo siku nne zilizopita lakini meneja wa ghala hiyo aliwataka kurejea nyumbani akisema hawakuwa na mbolea yoyote.
Walishangaa ni kwa nini walipokea ujumbe ukiwataka kufika ghalani hapo kuchukua mbolea.
Wakulima sasa wanaitaka serikali kufungua ghala katika maeneo bunge ili kufanya iwe rahisi kuchukua mbolea.
Walidai huku baadhi ya kaunti zikiwa zimepokea mbolea, hali ni tofauti katika kaunti ya Kericho.
Eric Rop ambaye ni meneja wa tawi la NCPB kaunti ya Kericho alisema ucheleweshwaji wa mbolea umesababishwa na matatizo ya kimfumo, suala linaloshuhudiwa kote nchini.
Alitoa wito kwa wakulima kuvuta subira wakati wakishughulikia suala hilo.