Mwenyekiti wa mamlaka ya kilimo na chakula nchini Cornelly Serem amesema kwamba Kenya hivi karibuni itaanza kuuza miraa nchini Israel baada ya kutambua wanunuzi nchini humo.
Kulingana na Serem hatua hii ni sehemu ya mpango wa kuongeza bidhaa za Kenya zinazouzwa Israel na kujaza ndege moja ya mizigo na bidhaa za Kenya zinazoelekea taifa hilo la mashariki ya kati.
Hivi maajuzi Serem aliongoza kundi la wajuzi hadi Israel kutafuta soko jipya na walifanikiwa.
Alikuwa akizungumza huko Meru wakati wa uzinduzi wa soko la kisasa la Miraa huko Muringene ambalo lilijengwa na serikali kuu.
Masoko engine kama hilo yanajengwa huko Laare na Tira.
Kenya imekuwa ikitegemea soko la Somalia pekee kwa uuzaji wa Miraa baada ya Uingereza kuipiga marufuku yapata miaka 10 iliyopita.
Wakulima wa miraa walipata pigo mwaka 2020 wakati soko la Somalia pia lilibania bidhaa hiyo lakini uuzaji wa Miraa huko Mogadishu ulirejelewa mwaka jana.
Wauzaji wa bidhaa hiyo hata hivyo wamewekewa kiwango cha Miraa ambacho wanaweza kuuza kila siku kutokana na hatua ya Mogadishu kupendelea bidhaa hiyo inayotoka Ethiopia.
Mbunge wa Igembe Kusini John Paul Mwirigi aliibua wasiwasi kwamba kulikuwa na kundi la wakiritimba ambalo linapanga kudhibiti soko la miraa nje ya nchi kwa kuweka bei.
Kufuatia hilo wauzaji wa bidhaa hiyo waliondolewa kwenye uwanja wa ndege mwaka jana kabla ya mamlaka ya kilimo na chakula pamoja na wizara ya kilimo kuingilia kati.