Baraza la Mawaziri limeidhinisha shilingi bilioni 4 zaidi kwa ajili ya wakulima wa kahawa nchini.
Hii inamaanisha wakulima sasa watapokea shilingi 80 kwa kila kilo moja ya kahawa kutoka shilingi 20 za sasa kama malipo ya mbeleni.
Fedha hizo ni nyongeza kwa shilingi bilioni 3 zilizotolewa awali.
Serikali pia itawatafutia wakulima masoko bora kimakusudi kwa kuwaalika wanunuzi maarufu wa kahawa kutoka kote duniani.
Hii italitia motisha Soko la Mauzo ya Kahawa la Nairobi ambalo limeshuhudia bei za chini na mauzo ya kiwango cha chini kwenye mnada.
Kadhalika, Baraza la Mawaziri limeidhinisha bajeti ya ziada inayojumuisha punguzo la asilimia 10 kutoka kwa wizara.
Hii inafuatia hatua ya serikali kuwianisha bajeti yake kwa kupunguza matumizi yasiyokuwa muhimu kama safari za nje ya nchi kwa zaidi ya shilingi bilioni 71.
Na kama sehemu ya Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Usalama kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Mawaziri pia liliidhinisha upelekwaji wa maafisa wa polisi nchini Haiti kama ilivyokubaliwa na Baraza la Kitaifa la Usalama.
Azimio la Baraza la Kitaifa la Usalama kuhusiana na upelekwaji wa maafisa hao limewasilishwa bungeni ili kuidhinishwa kwa mujibu wa kifungu 240 cha katiba.