Wakulima wa kahawa kutoka chama cha Othaya kuanza kupokea malipo

Tom Mathinji
1 Min Read
Serikali kuongeza kiwango cha kahawa kinachouzwa nje ya nchi.

Zaidi ya wakulima 10,000 wa kahawa kutoka chama cha ushirika cha Othaya, wanasababu ya kutabasamu kwani wataanza kupokea malipo kutokana na kahawa walichowasilisha katika kipindi cha upanzi cha mwaka 2023/2024.

Mwenyekiti wa chama hicho James Gathua, alisema licha ya kupungua kwa uzalishaji wakati wa kipindi cha mwaka 2023/2024, wakulima hao watapata malipo yaliyoimarika kutokana na mauzo bora ya msimu huu ikilinganishwa na msimu uliopita.

Kulingana na ratiba ya malipo kutoka chama hicho, wakulima hao watapokea shilingi 105.15 kwa kila kilo moja iliyowasilishwa.

Malipo hayo kulingana na Gathua, yanaashiria ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na malipo ya msimu wa upanzi wa mwaka 2022/2023, ambapo wakulima walilipwa shilingi 83.15 kwa kila kilo la kahawa walilowasilisha.

“Msimu uliopita, tulizalisha kilo 2,316,539 ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2022/2023 ambapo kilo 3,572,982 zilizalishwa. Upungufu huo wa uzalishaji ulisababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na magonjwa,” alisema Gathua.

Gathua alisema chama hicho kimeanza kuwapiga jeki wakulima kuimarisha ubora wa zao hilo, huku wakijiandaa kwa msimu ujao wa upanzi.

“Tumeandaa warsha ya kutoa mafunzo kwa wakulima, na pia tumewaajiri wataalam wawili watakao watembelea wakulima na kuwapa ushauri,” alisema mwenyekiti huyo.

Website |  + posts
Share This Article