Wakulima 4,000 wapokea mbegu za alizeti kaunti ya Nakuru

Tom Mathinji
1 Min Read

Wakulima 4,000 kaunti ya Nakuru wamepokea mbegu zilizoidhinishwa za alizeti kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo, katika hatua za kuongeza uzalishaji wa bidhaa za mafuta ya kupikia.  

Hatua hiyo inalenga kupunguza uagizaji mafuta ya kupikia kutoka nchi za kigeni, na hivyo kupunguza gharama ya mafuta ya kupikia hapa nchini.

Afisa wa mimea wa kaunti ya Nakuru Lilian Samoei, alisema mbegu hizo zilisambazwa kwa wakulima waliosajiliwa, ambapo kilo 15,000 zilikusudiwa kupandwa katika ekari 5,000 za ardhi katika kaunti hiyo.

Huku akidokeza kuwa Kenya hutumia shilingi bilioni 160 kila mwaka kuagiza mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi, afisa huyo alisema serikali ya Gavana Susan kihika imeazimia kupiga jekiuzalishaji wa alizeti ili kusaidia kupunguza gharama ya bei ya mafuta ya kupikia hapa nchini.

“Tunapigia debe uzalishaji wa alizeti, kuhakikisha wakulima wanafaidika kifedha,” alisema Samoei.

Aliyasema hayo katika wadi ya Nyota, kaunti ndogo ya Kuresoi Kaskazini wakati wa hafla ya kupigia debe uzalishaji wa alizeti.

Kulingana na takwimu kutoka halmashauri ya chakula na kilimo AFA, Kenya huzalisha asilimia 34 ya mafuta ya kupikia, huku nakisi ikiagizwa kutoka mataifa ya nje.

TAGGED:
Share This Article