Wakili wa Besigye ahukumiwa kifungo cha miezi 9 gerezani

Alihukumiwa kutokana na kile kinachotajwa kuwa kudharau mahakama.

Marion Bosire
2 Min Read
Eron Kiiza, Wakili, Uganda

Wakili wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye, Eron Kiiza amehukumiwa kifungo cha miezi tisa gerezani na mahakama ya kijeshi ya Makindye nchini Uganda.

Hii ni baada ya mahakama hiyo kumpata na hatia ya kudharau mahakama.

Alikamatwa mapema leo katika mahakama hiyo hiyo wakati yeye na mawakili wengine wa Besigye walikuwa wakishinikiza waruhusiwe kuingia mahakamani.

Baadaye alasiri, Kiiza alirejeshwa kwenye mahakama hiyo na kuhukumiwa kifungo hicho bila kusomewa mashtaka na bila kupatiwa fursa ya kujitetea.

Robert Kyagulanyi ambaye pia ni kiongozi wa upinzani nchini Uganda, anaonekana kughadhabishwa na matukio hayo akisema kosa pekee alilolifanya Kiiza ni kusisitiza haja ya kuruhusiwa kufanya kazi yake.

“Kosa lake ni kusisitiza kuruhusiwa kutekeleza kazi yake kama wakili, kuwakilisha wateja wake, baada ya kuzuiwa kufanya hivyo.” ameandika Kyagulanyi kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanamuziki anahimiza watu wa Uganda kuungana kupambana na kile alichokielezea kuwa hali inayozidi kuzorota.

Mawakili wengine wa Kizza Besigye na msaidizi wake Obeid Lutale wakiongozwa na Martha Karua na Meya wa Kampala Erias Lukwago walikataa kuendelea na kesi hiyo bila wakili Kiiza.

Walipatiwa dakika 15 kujadiliana na kuamua hatima ya kesi hiyo na walishikilia msimamo wao wakisema wateja wao wanataka wawakilishwe na mawakili wote jinsi walikuwa wamepanga.

Walisisitiza pia kwamba Wakili Kiiza ana mawasilisho muhimu katika kesi hiyo.

Mahakama iliamua kwamba Kizza na Lutale watarejea humo januari 13, 2025.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *