Wakfu wa Ford watakiwa kutoa maelezo kuhusu mashirika inayofadhili

Tom Mathinji
2 Min Read
Katibu katika wizara ya Mambo ya Nje Korir Sing'Oei.

Serikali ya Kenya siku ya Jumatano iliiandikia wakfu wa Ford, kuhusu uwezekano wa baadhi ya mashirika inayofadhili kujihusisha katika maandamano ya hivi punde dhidi ya serikali.

Katika barua hiyo, katibu katika wizara ya mambo ya nje Dkt. Korir Sing’Oei, alidokeza kuwa serikali ya Kenya inawasiwasi kwamba wanaofadhiliwa na wakfu wa Ford, huenda walihusika katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, wakitumia fedha za wakfu huo kusambaratisha amani na usalama hapa nchini.

“Ifahamike kwamba baadhi ya mashirika yanayofadhiliwa na wakfu wa Ford, yalipokea dola Milioni 5.78 ambazo ni sawa na shilingi Milioni 752 kati ya Mwezi Aprili mwaka 2023 na mwezi mei mwaka 2024, huku shilingi milioni 194 kati ya fedha hizo zikiwa hazina maelezo ya jinsi zilivyotumika,” alisema Sing’Oei.

Kulingana na katibu huyo, fedha hizo zilizotumwa kwa mashirika hayo yasiyokuwa ya serikali, zinapaswa kutumiwa vyema kulingana na malengo yaliyokusudiwa, la sivyo yatafujwa kufadhili uhalifu.

“Baadhi ya mashirika mnayofadhili, yanakiuka sheria za Kenya, ikiwa ni pamoja na zile zinazozuia uchochezi, semi za chuki na uenezaji habari za uwongo,” alidokeza Sing’Oei.

Sing’Oei aliorodhesha mashirika 16 yanayohudumu hapa nchini na jinsi yalivyopokea fedha kutoka kwa wakfu wa Ford.

Mashirika hayo ni pamoja na:

  1. Africa Uncensored Limited (Project Mulika) (US$ 250,000).
  2. Women’s Link Worldwide; (US$ 750,000).
  3. Centre for Resource Mobilization and Development; (US$ 20,000),
  4. Transform Empowerment for Action Initiative: (US$ 220,000),
  5. Kenya Human Rights Commission (US$ 600,000),
  6. Open Institute Trust; (the US $100,000),
  7. Africa Centre for Open Governance: (US$ 200,000),
  8. Transparency International: (US$ 300,000),
  9. The Institute for Social Accountability (TISA) (US$ 200,000),
  10. National Coalition of Human Rights Defenders (K); (US$ 257,000),
  11. Shinning Hope for Communities Inc. (US$2,050,000),
  12. Coalition for Grassroots Human Rights Defenders Kenya (US$ 250,000),
  13. Community Aid International (US$ 100,000),
  14. Mzalendo Trust; (US$ 335,000),
  15. Usikimye (Femicide); (US$ 30,000),
  16. Citizens Advancement Initiative; (US$ 150,000).

Taifa hili limeshuhudia wimbi la maandamano hivi majuzi yaliyoongozwa na vijana wa Gen Z, yaliyosababisha Rais William Ruto kuvunja Baraza la Mawaziri na kufanya mabadiliko katika huduma ya taifa ya polisi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *