Wakenya watakiwa kuwa waangalifu kuepusha maafa msimu huu wa sherehe

Martin Mwanje
2 Min Read

Serikali imewataka Wakenya kuzingatia sheria za barabarani kikamilifu na kuwa waangalifu zaidi ili kuepusha vifo na majeraha yanayotokana na ajali za barabarani hasa wakati huu wa msimu wa sherehe. 

Kwa kawaida, ajali nyingi hushuhudiwa mwezi Disemba wakati idadi kubwa ya watu huwa wanasafiri.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi anasema kufikia sasa, idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini imepungua ikilinganishwa na mwaka 2023.

Kulingana naye, idadi ya vifo miongoni mwa madereva imepungua kwa asilimia 5.85, abiria (10%), abiria wanaokaa nyuma (9%) na waendeshaji pikipiki asilimia 10.05.

Hata hivyo, akiwahutubia wanahabari leo Alhamisi, Mudavadi ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Usalama wa Taifa amesema idadi ya abiria wanaojeruhiwa vibaya kutokana na ajali za barabarani imeongezeka kwa karibu asilimia 11 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Huku msimu wa sherehe za Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya ukipamba moto, Waziri huyo amewataka Wakenya wote kuchukua tahadhari ili kuepusha maafa zaidi.

“Mwezi wa Disemba kwa kawaida hurekodi idadi kubwa zaidi ya vifo. Kwa hivyo, natoa wito kwa Wakenya wakati huu wa msimu wa sherehe hasa madereva wa magari ya usafiri wa umma wanaoendesha magari ya masafa marefu kuwa waangalifu na kuendesha magari kwa njia salama,” alisihi Mudavadi aliyekuwa ameandamana na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo miongoni mwa maafisa wengine wakuu serikalini.

Kadhalika, ameaagiza kuongezwa kwa maafisa wa polisi wanaoshika doria kwenye barabara kuu usiku na mchana ili kuhakikisha sheria zote za barabarani zinazingatiwa.

Maafisa wa polisi pia wametakiwa kuhakikisha ni magari tu yaliyo katika hali nzuri yanasafiri na ni lazima yawe na leseni zinazohitajika.

Uendeshaji wa magari kwa kasi pia umepigwa marufuku.

Serikali inalenga kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 50 kabla ya mwaka 2028.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *