Wito umetolewa kwa Wakenya kuishi kwa amani na kuwakatalia mbali viongozi wanaowaganywa kwa misingi ya kikabila.
Wito huo umetolewa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na mwenzake wa Bunge la Seneti Amason Kingi wakati wakizungumza wakati wa mazishi ya mama yake mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, Dorothy Baya Mweri.
Viongozi hao pia wamewataka viongozi waliochaguliwa kutoka eneo la Pwani kuelezea mafanikio ya maendeleo yaliyoafikiwa na serikali ya Kenya Kwanza kama njia ya kuinadi serikali hiyo kwa wapiga kura.
Wetang’ula akitumia fursa hiyo kuonya dhidi ya juhudi za kuwachochea Wakenya akisema hiyo siyo suluhu kwa changamoto zinazolikumba taifa kama vile gharama ya maisha na ukosefu wa ajira.
Kwa upande wake, Kingi alisema viongozi wa eneo la Pwani wanamuunga mkono Rais William Ruto ila hawajakuwa mstari wa mbele kuwaambia wakazi miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali yake.
Aliwataka kubadili dira hiyo na kuelezea wakazi miradi ya maendeleo inayofanywa na utawala wa Kenya Kwanza katika eneo hilo kwa manufaa yao.
Taarifa hii imechangiwa na Dickson Wekesa