Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa Wakenya kuwajibika na kuchukua tahadhari wakati wa mvua za El Nino zinazoendelea nchini.
Mvua hizo zimesababisha vifo vya watu 87 na familia 35,000 kuachwa bila makazi.
Akiwatakaa Wakenya kukoma kufanya masihara na mvua hizo, Gachagua alisema kati ya vifo vilivyosababishwa na mvua hizo, 37 vilitokana na kuzama kwa watu waliojaribu kuvuka mito iliyofurika.
“Tunatoa wito kwa Wakenya kuwajibika na kuchukua tahadhari hata wanapotoa wito kwa serikali kuingilia kati. Angalau vifo 37 vilivyosababishwa na mvua za El Nino vilitokana na watu kuzama na watu kuthubutu mvua hizo. Kuna watu wanaovuka mito wakati wanaweza wakaona maji ni mengi na ya kutisha. Wanasisitiza kuwa wana mbio za kwenda mahali,” alisema Gachagua wakati akifungua Mkutano wa 17 wa kila mwaka wa Taasisi ya Wapangaji Nchini katika hoteli ya Diani Reef.
“Natoa wito kwa Wakenya kuwajibika na kutunza maisha yao, tusiwe watu wa kuthubutu. Tumezitaka timu za usalama za kaunti kuwasaidia Wakenya katika kuweka hatua za kuhakikisha watu hawahatarishi maisha yao.”
Alisema serikali imeweka hatua za kukabiliana na mafuriko na kuhakikisha hakuna vifo zaidi vitakavyotokea kutokana na mafuriko na watu kupoteza vitega uchumi vyao.