Wakenya watakiwa kusherehekea Pasaka kwa kuwajibika

Martin Mwanje
1 Min Read

Mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi ametoa wito kwa Wakenya kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kuwajibika na kutenga muda ili kusherehekea na familia zao. 

Katika ujumbe wake wa Pasaka, Dorcas alisema sherehe za Pasaka ni wakati mzuri wa familia kuwa pamoja.

“Mnapoenda kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, hakikisheni kuwa mnawajibika. Kina baba watunzeni watoto wenu, wanaume watunzeni wanawake wenu, wanawake wapendeni wanaume wenu na mhakikishe Pasaka hii itakuwa wakati ambao tutasherehekea pamoja kama familia,” alisihi Dorcas.

Aliongeza kuwa sherehe za Pasaka ni wakati wa taadhima kwa Wakristo kote duniani na kwa hivyo wanapaswa kuchukua muda kuwazia kifo na kufufuka kwa Yesu Kristo.

“Pasaka ni wakati wa taadhima kwa Wakristo kwa sababu huu ni wakati ambapo Wakristo wanafahamu kwamba wao ni kiumbe kipya, wanafahamu kwamba wana uzima wa milele.”

Wakati wa sherehe hizo, Dorcas alitoa wito kwa Wakristo kuwakumbuka wale wanaohisi wamekataliwa, kuwatembelea wajane, mayatima, wale wanaoishi na ulemavu na watu kama hao wasiojiweza na kuwapa sababu ya kusherehekea.

Website |  + posts
Share This Article