Rais William Ruto amewataja Wakenya wanaoishi ughaibuni kuwa mnara wa kutia moyo kwa Kenya na dunia nzima kwa jumla.
Akirejelea wajibu mkubwa na mchango unaotolewa na Wakenya hasa katika kuhakikisha ustawi wa nchi, Ruto alitaja uzalendo, uchapaji kazi kwa bidii, ubunifu na kudhamiria kunawiri kazini kuwa nguvu ya mafanikio na maono ya ustawi wa pamoja.
“Sina shaka katika uwezo wenu kama watu wetu wanaoishi na kufanya kazi hapa, kwa sababu najua Wakenya wanaoishi ng’ambo kwa muda mrefu wamekuwa mnara wa kutia moyo, wakionyesha dhamira isiyoyumba kwa ukuaji wa nchi yetu,” alisema Rais Ruto.
Aliyasema hayo jana Jumanne jioni mjini Accra alipokutana na Wakenya wanaoishi nchini Ghana. Ruto anafanya ziara ya siku tatu nchini humo.
“Kazi yenu ya bidii, ubunifu na kujitolea kunawiri kazini siyo tu imehakakikisha ufanisi wetu binafsi lakini pia umetoa mchango chanya nchini Kenya na duniani.”