Wakenya watalenga kuendeleza ubabe wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa vidosho leo usiku, huku makala ya 20 ya mashindano ya riadha ya Dunia kwa chipukizi chini ya umri wa 20 yakiingia siku tatu mjini Lima Peru.
Sharon Chepkemoi na Diana Chepkemoi watashiriki fainali hiyo kuanzia saa saba na dakika 27 usiku, huku Kenya ikijivunia kutwaa ubingwa mara tisa kati ya makala 10 tangu kujumusihwa kwa shindano hilo mwaka 2006.
Baadaye Dennis Koech na Clinton Kimutai watatimka fainali ya mita 3,000 kuanzia saa nane na daika 17 usiku wa manane.
Bingwa wa Afrika Sarah Moraa, Kelvin Kimutai, na Phanuel Koech pia watarejea uwanjani katika nusu fainali ya mita 800.
Mercy Chepkemoi aliyemaliza wa nne katika fainali ya mita 5,000 atashirikiana na Marion Jepng’etich katika mchujo wa mita 3,000.
Wakenya watatu walifuzu kwa fainali ya mita 1,500 jana usiku wakiwa ,Josphat Kipkurui ,Mary Nyaboke na Miriam Chemutai.
Bingwa wa Afrika Sarah Moraa,Phanuel Koech na Kelvin kimutai watatimka nusu fainali ya mita 800 leo usiku.
Mapema leo Alana Reid wa Jamaica na Bayanda Walaza wa Afrika Kusini walitwaa ubingwa katika mita 100 kwa wanawake na wanaume mtawalia.
Reid alishinda dhahabu kwa sekunde 11.17 akifuatwa na Hodge Adaeja wa visiwa vya British Virgin aliyenyakua fedha huku Kishawna Nile wa Baarbados akiridhia shaba.
Walaza alishinda dhahabu ya wanaume kwa kufyatuka kwa sekunde 10.19 akifuatwa na Boonson Puripol wa Thailand na Bradely Nkoana walioshinda fedha na shaba mtawalia.
Kenya ni ya tano kwenye msimamo wa dunia kwa dhahbu moja iliyotwaliwa na Adrew Alamisi Kiptoo katika fainali ya mita 5,000.
Australia inaongoza kwa dhahabu 2 na shaba moja ikifuatwa na Ethiopia kwa dhahabu 1 na fedha 2 huku China na Afrika Kusini zikishikilia nafasi ya tatu kwa pamoja zikiwa na dhahabu moja ,fedha moja na shaba moja kila moja.
Mashindano hayo yanayoandaliwa Amerika Kusini kwa mara ya pili mtawalia yatakamilika Jumamosi hii.