Wakenya wahimizwa kuwa na subira

Marion Bosire
1 Min Read
Johnson sakaja, Gavana Nairobi

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja amehimiza wakenya wawe na subira na wampatie Rais William Ruto muda wa kutekeleza ahadi alizotoa.

Akizungumza katika kanisa katoliki la Soweto kaunti ya Nairobi ambako aliandamana na Rais Ruto kwa ibada, Sakaja alisema kwamba ruto amekuwa uongozini kwa miaka miwili pekee.

Kulingana naye, viongozi wa awali walichukua muda kabla ya kuafikia maendeleo na sio miaka miwili tu.

Alitoa mfano wa serikali ya hayati Mwai Kibaki ambayo ilijenga barabara kuu ya Thika Road kwa mwaka wa tano huku serikali ya Uhuru Kenyatta ikijenga barabara ya Expressway mwaka wa tisa uongozini.

“Imekuwa miaka miwili tu na lawama zote zinaelekezwa kwa Rais Ruto. Miaka miwili atatue shida za miaka 60.” alisema Sakaja akiongeza kwamba aliyejaliwa mengi anatarajiwa kutekeleza mengi vile vile.

Sakaja alimsifia Rais Ruto kwa utendakazi wake akisema umahiri wake ndio unasababisha aharakishwe na wananchi kutekeleza maendeleo.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya maaskofu wa kanisa katoliki nchini kutoa taarifa ya pamoja wakidai uwajibikaji kutoka kwa serikali.

Akizungumza jana huko Embu, katika hafla ya kutawazwa kwa askofu wa kanisa katoliki, Rais aliahidi kushughulikia masuala yote yaliyoibuliwa na maaskofu wa kanisa katoliki.

Website |  + posts
Share This Article