Mkuu wa utumishi wa umma Felix Felix Koskei, amehimiza wakenya kukumbatia mavazi ya ujana kuanzia kesho hadi sikukuu ya Jamhuri Disemba 12, 2023 wakati Kenya itakuwa inaadhimisha miaka 60 ya kujitawala.
“Kuanzia kesho jadi sikukuu ya Jamhuri, tukumbatie mavazi ya kawaida yanayoonekana vizuri tukilenga kushabikia kongamano la vijana barani Afrika almaarufu “Africa YouthConnekt Summit” aliandika Koskei kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Koskei anahimiza wakenya kuonyesha kwamba wanaunga mkono vijana na kongamano lao kwa kuvaa jezi za timu za Kenya au za Afrika ambazo wanapenda kama vile za wanariadha, za timu ya taifa ya soka Harambee Stars, timu ya Shujaa au ile ya Malkia Strikers.
Kongamano hilo la vijana linaandaliwa jijini Nairobi nchini Kenya kati ya Disemba 8 na 11, 2023 na hii ni awamu ya 6.
Waandalizi wa kongamano hilo ni serikali ya Kenya kwa ushirikiano na kituo cha YouthConnekt Africa na shirika la umoja wa mataifa kuhusu maendeleo, UNDP.
Vijana wapatao elfu 20,000, wawakilishi wa serikali, viongozi wa sekta ya kibinafsi na mabingwa wa maendeleo barani Afrika wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo.
Litaangazia uongozi wa vijana na uvumbuzi kwa ajili ya ujumuishaji wa Afrika kupitia kwa mazungumzo kuhusu sera, simulizi na mitandao na mipango inayolenga wafanyabiashara ikiwemo mikutano na wawekezaji.