Wakenya tayari kwa makabiliano ya mbio za dunia za barabarani

Dismas Otuke
2 Min Read

Wanariadha wa Kenya watashiriki makala ya kwanza ya mbio za dunia za barabarani, zitakazoandaliwa mjini Riga nchini Latvia siku ya Jumapili.

Bingwa mtetezi wa mashindano ya mbio za dunia za nusu marathon Peres Jepchirchir atakuwa akitetea taji yake ya mwaka uliopita huku wakishikiriana na Irene Kimais,Margaret Chelimo na Catherine Relin.

Kimais akizungumza na KBC alipokuwa akiondoka alikuwa mwingi wa matumaini ya kufanya vyema licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza.

“Nimejiandaa vizuri na ninataka nikimbie vizuri hata kama ndio mara yangu ya kwanza naomba Wakenya watusupport.”akasema Kimais

Katika mbio za wanaume za nusu marathon mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mita mita 5,000 Daniel Simiu anaangazia kujiongezea mishani nyingine.

“Najua haitakuwa rahisi lakini nitajikaza ,natarajia upinzani kutoka kwa Kiplimo wa Uganda na wengine tuliokuwa nao Budapest.”akasema Simiu

Mwingine katika timu ya nusu marathon ni Sebastien Sawe bingwa wa Berlin half marathon.

“Nafurahia kuenda kushiriki kwa mara ya kwanza na ninaahidi Wakenya nitaleta mazuri.”akasema Sawe

Charles Kipkurui, Samwel Nyamai,na Benard Kibet ndio washiriki wengine wa nusu marathon.

Washiriki wa mbio za umbali wa maili moja ni:- Reynold Kipkorir Cheruiyot, Nelly Chepchirchir, Beatrice Chepkoech na bingwa mara tatu wa dunia katika mita 1500 Faith Kipyegon.

Katika mbio za kilomita tano, wanariadha watakaotimka ni:- Cornelius Kemboi, Nicholas Kipkorir, Stanley Waithaka, bingwa wa dunia wa mbio za nyika Beatrice Chebet, Caroline Nyaga na Lilian Kasait.

Kenya itawakilishwa na wanariadha 21, wanaume 10 na wanawake 11, wengi wao wakiwa wale walioshiriki mashindano ya dunia mjini Budapest nchini Hungary mwezi uliopita.

Share This Article