Wakenya milioni 33.7 wamejisajili SHA, asema Ruto

Martin Mwanje
1 Min Read

Jumla ya Wakenya milioni 33.7 wamejisajili na Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA. 

Rais William Ruto amesema hii ni kinyume cha Wakenya wapatao milioni 8 waliokuwa wamejisajili na iliyokuwa bima ya afya ya NHIF miaka minne iliyopita.

“Lakini umuhimu wa mageuzi haya unazidi takwimu za waliojisajili,” alisema Rais Ruto wakati akihutubia taifa kutoka majengo ya bunge.

“Unajikita kwenye matibabu ambayo familia zinaweza zikayapata na bili za matibabu ambazo hawahitajiki kulipa peke yao.”

Ruto alisema kote nchini, wagonjwa 53,465 wanapokea matibabu ya saratani huku wagonjwa 24,468 wakisafishwa damu kwa mashine ya figo.

Wagonjwa 89 tayari wamepandikiziwa figo chini ya mfumo mpya wa SHA, aliongeza Rais, akisema huduma hizo ambazo zinapatikana chini ya SHA ni ghali mno kwa mgonjwa binafsi kugharimia.

Ruto alikiri kuwa mfumo wa SHA umekumbwa na changamoto katika utekelezaji wake tangu kuasisiwa kwake lakini serikali imejizatiti kuzishughulikia kwa manufaa ya wagonjwa wanaotafuta matibabu chini ya mfumo huo.

 

 

 

 

Share This Article