Wakenya leo Jumamosi wataweza kuzuru bila malipo mbuga na hifadhi za wanyamapori kote nchini kama sehemu ya maadhimisho ya juma la kimataifa la utalii.
Hayo yanafuatia tangazo la waziri wa utalii Rebecca Miano, ambaye aliwataka wakenya kutumia fursa hiyo kuzuru mbuga na hifadhi hizo za wanyama pori.
Miano alisema hatua hiyo ni njia moja ya kuwarudishia shukrani wakenya kwa juhudi zao za kuhifadhi wanyama pori.
Wakati huo huo, waziri huyo alitoa wito wa juhudi za pamoja katika kutumia uwezo wa sekta ya utalii kukuza amani na umoja katika jamii.
Waziri alisema utamaduni ni nguzo muhimu katika kukuza amani, uwiano na maendeleo endelevu. Miano aliwataka wadau kutumia fursa ya mageuzi yanayoendelea katika sekta ya utalii kuchangia ustawi wa taifa na umoja miongoni mwa jamii mbali mbali.
Kwa upande wake, gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Olentutu, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya baraza la Magavana kuhusu utalii na uhifadhi wa wanyama wa pori, aligusia umuhimu wa kuendeleza utalii katika ngazi ya Kaunti.
Alisema Kaunti nyingi humu nchini zimebarikiwa na aina mbali-mbali za vivutio vya kitalii.