Wakenya wataanza kumiliki nyumba zilizojengwa chini ya mpango wa gharama nafuu kufikia mwishoni mwa mwaka huu, hayo ni kulingana na msemaji wa serikali Isaac Mwaura.
Mwaura alisema ujenzi wa nyumba kadhaa unakaribia kukamilika, na katika muda wa miezi michache ijayo, zitakuwa tayari kwa makazi.
Akizungumza mjini Ruiru kaunti ya Kiambu alipokuwa akikagua ujenzi wa nyumba 1,050, Mwaura alisema nyumba hizo ni za kisasa, huku vifaa muhimu vikiwekwa tayari kwa makazi.
“Hitaji la nyumba hizi ni la juu na tunashikilia kuwa uuzaji wa nyumba hizi utatekelezwa kwa njia iliyo wazi na usawa. Wale walio na matatizo ya makazi watapewa kipaumbele. Nyumba hizi zenye vyumba viwili na vitatu vya malazi, zitauzwa kwa shilingi milioni 1.2 hadi shilingi milioni 4.5,” alisema Mwaura.
Kulingana na Mwaura mpango huo wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, umechangia pakubwa kwa ukuaji wa uchumi kote nchini, kupitia nafasi za ajira zilizobuniwa na kupigwa jeki kwa biashara za maeneo hayo.
“Kwa mfano katika mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu hapa Ruiru, wakazi 1,300 wamepata ajira huku biashara za eneo hili zikifaidika kutokana na ununuzi wa mali ghafi kama vile, vyuma, mchanga na saruji,” alisema msemaji huyo wa serikali.