Wakenya watalazimika kugharimika zaidi baada ya kupanda kwa bei za mafuta katika tathmini mpya iliyotangazwa na Halmashauri ya Kudhibiti Bei za Nishati na Mafuta, EPRA Alhamisi usiku.
Bei hizo mpya za mafuta zitatekelezwa kuanzia Septemba 15, usiku wa manane hadi Oktoba 14, 2023.
Katika taarifa iliyotolewa na halmashauri hiyo ikiashiria ongezeko kubwa la bei za mafuta nchini, lita moja ya mafuta ya petroli jijini Nairobi sasa itauzwa kwa shilingi 211.64 baada ya kuongezwa kwa shilingi 16.96, lita moja ya dizeli itauzwa kwa shilingi 200.99 baada ya kuongezwa kwa shilingi 21.32 wakati mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 202.61 kwa lita baada ya kuongezwa kwa shilingi 33.13.
Jijini Mombasa, mafuta ya petroli sasa yatauzwa kwa shilingi 208.58 kwa lita, dizeli shilingi 197.93 wakati mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 199.54 kwa lita.
Jijini Kisumu, wakazi watalazimika kuzamia zaidi na kununua mafuta ya petroli kwa shilingi 211.40 kwa lita wakati yale ya dizeli yakiuzwa kwa shilingi 201.16 kwa lita. Mafuta taa jijini humo yatauzwa kwa shilingi 202.77 kwa lita.
Jijini Kakamega, mafuta ya petroli yatauzwa kwa shilingi 211.45 kwa lita, dizeli shilingi 201.21 huku mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 202.83 kwa lita.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Bargoria, ongezeko hilo linatokana na ongezeko la kufikisha mafuta yaliyoagizwa nchini ambapo gharama za kusafirisha mafuta ya petroli hadi Mombasa ziliongezeka kwa asilimia 4.80, mafuta ya dizeli kwa asilimia 12.52 na mafuta taa kwa asilimia 19.79.