Wakenya watalazimika kugharimika zaidi baada ya mamlaka ya kudhibiti bei za mafuta, EPRA kuongeza bei siku ya Jumamosi.
Kulingana na taarifa, EPRA imeongeza bei ya petroli kwa shilingi 5 na senti 72 kwa lita moja, bei mpya ya bidhaa hiyo kaunti ya Nairobi ikiwa shilingi 217 na senti 36.
Dizeli imeongezwa kwa shilingi 4 na senti 48 na sasa itauzwa kwa shilingi 205 na senti 47 kwa kila lita moja, wakati mafuta taa yakipandishwa kwa shilingi 2 na senti 45 na sasa bei mpya katika kaunti ya Nairobi itakuwa shilingi 205 na senti 06 kwa kila lita moja.
EPRA imesema bei hiyo ingepanda zaidi endapo serikali haingeweka mikakati ya kudhibiti bei kupitia kwa hazina ya ushuru wa petroli, PDL .