Wakenya wabanwa zaidi baada ya matatu kuongeza nauli

Dismas Otuke
1 Min Read

Wakenya watalazimika kukabiliana na makali ya hali ngumu ya kiuchumi na gharama ya juu ya maisha, baada ya wenye matatu kutangaza kuongeza nauli za usafiri katika kaunti ya Nairobi. 

Kulingana na chama cha wamiliki wa matatu, MOA bei mpya ya usafiri imeongezwa kwa shilingi 50 nyakati za asubuhi na jioni wakati kuna abiria wengi huku nyakati zisizo na abiria wengi, nauli ikiongezwa kwa shlingi 30.

Chama cha MOA kimeafikia uamuzi huo kufuatia kuongezwa kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli kulikotangazwa na halmashauri inayodhibiti bei ya mafuta, EPRA Alhamisi usiku.

Bei ya mafuta ya petroli  iliongezwa kwa shilingi 16.97 kwa kila lita moja na kupita shilingi 200 huku dizeli ikiongoezwa kwa shilingi 21.32 kwa lita katika kaunti ya Nairobi.

Bei hizo zimeanza kutekelezwa mara moja.

Share This Article