Wakazi wa Samburu waonywa dhidi ya ukeketaji wasichana

Tom Mathinji
1 Min Read
Kaimu naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Samburu Mashariki, James Katana.

Wakazi wa kaunti ndogo ya Samburu Mashariki wameonywa dhidi ya kuendeleza tamaduni potovu ya ukeketaji wa wasichana.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa ufadhili wa masomo kwa zaidi ya wasichana 150 kutoka eneo la Ngilai ya Kati, kaimu naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Samburu Mashariki James Katana  alisema yeyote atakayepatikana akipanga ama kutekeleza tamaduni hiyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Natoa agizo kwa machifu na wazee wa eneo hili kwamba mkipata habari kuhusu mtu yeyote anayepanga kutekeleza uovu huo dhidi ya mtoto, mnipashe habari mapema ili mtu kama huyo tumchukulie hatua za kisheria,”alifoka Katana.

Aidha, Katana amewahimiza wakazi hao kuwapeleka watoto wao shuleni, akidokeza kuwa ni kupitia kwa elimu, ndipo jamii hiyo itaimarika.

Mradi huo wa ufadhili wa masomo almaarufu Sampiripiri, unalenga kuongeza idadi ya wanawake walio na elimu na kuwawezesha kukabiliana na ndoa za mapema katika eneo hilo la Wamba.

Kulingana na Katana, wasichana hao watanufaika na rasilimali za kijamii kama vile maeneo salama, lishe bora, huduma bora za afya na kiuchumi pamoja na usawa wa kijinsia.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *