Wakazi wa Rumuruti waandamana kupinga ujenzi wa kituo cha kurekebisha tabia

Marion Bosire
2 Min Read
Wakazi wa Rumuruti wakiandamana

Baadhi ya wakazi wa mji wa Rumuruti katika kaunti ya Laikipia wamepinga ujenzi uliopangwa wa kituo cha matibabu na urekebishaji tabia ambacho kilizinduliwa hivi maajuzi na mke wa naibu Rais mhubiri Dorcas Rigathi, katika eneo hilo.

Wakazi hao walifanya maandamano ya amani mjini humo leo wakilalamika kwamba umma haukushirikishwa kabla ya wazo la kujenga kituo hicho kwenye ardhi ya ekari 301 katika eneo hilo kuafikiwa.

Wanailaumu serikali ya kaunti ya Laikipia kwa kutoa ardhi hiyo kwa mradi husika ilhali kulikuwa na pendekezo la awali lililoidhinishwa kwa mradi huo wa kituo cha urekebishaji tabia kulingana na ushirikishi wa umma kufuatia taarifa iliyochapishwa kwenye magazeti ya humu nchini Novemba 4, 2021.

Wakati wa kuanzisha ujenzi wa kituo hicho katika eneo la Kandutura mwezi uliopita, mhubiri Dorcas alisema afisi yake itashirikiana na idara ya mahakama na serikali ya kaunti ya Laikipia kujenga kituo hicho ambacho pia kitatumika kama eneo la kuzuilia wanaokosa.

Solomon Mwangi, mkazi wa eneo hilo alisema kwamba chini ya mpango wa mji wa Rumuruti wa mwaka 2021 hadi 2031, umma ulikuwa umetoa ardhi ya kujenga kituo hicho, ardhi ambayo haijatumika hadi sasa, na sasa kituo hicho kimetengewa ardhi tofauti na serikali ya kaunti.

Kulingana naye ardhi ya ekari 301 ambayo inalengwa kwa ujenzi wa kituo hicho haijawahi kuzungumziwa kwenye kikao chochote cha ushirikishi wa umma.

Serikali ya kaunti sasa inaombwa kusitisha shughuli zote kwenye ardhi hiyo na iharakishe mchakato wa kugawia maskwota ardhi kwenye eneo la Kandutura settlement scheme.

Wakazi hao wametishia kuandaa maandamano kila wiki na kulemaza shughuli za soko maarufu la mifugo la Rumuruti hadi pale ambapo matakwa yao yatashugulikiwa.

Share This Article