Naibu Rais Kithure Kindiki amehakikishia wakazi wa kaunti ya Narok, kwamba utawala wa Rais William Ruto, umejitolea kuhakikisha maendeleo sawa katika sehemu zote za nchi.
Akizungumza katika mkutano wa uwezeshaji kiuchumi katika eneo la Kojong’a, Narok Mashariki, Kindiki alisisitiza kwamba hakuna eneo litakaloachwa nyuma kimaendeleo kwa misingi ya miegemeo ya kisiasa na kabila.
Kindiki alisema kwamba kila kiongozi aliyechaguliwa kote nchini yuko serikalini na Kenya ina Rais mmoja ambaye anahudumia wananchi wote kwa usawa bila kuzingatia waliyempigia kura wakati wa uchaguzi.
Naibu huyo wa Rais alikumbusha wakazi wa Narok kwamba Kenya ni nchi moja, iliyo na bendera moja na watu wenye umoja.
Kiongozi huyo aliwataka viongozi wa upinzani wawasilishe ajenda yao ya maendeleo pamoja na mipango ya maendeleo kwa wakenya wanapojipigia debe badala ya kujihusisha na siasa za ukabila.
Kulingana naye serikali tayari imeangazia ajenda yake ya maendeleo inayohusisha ujenzi wa masoko ya kisasa, barabara, shule, uunganishaji umeme na uwezeshaji kiuchumi.
Kindiki aliupa upinzani changamoto ya kujadiliana na serikali kwa njia ya utulivu na kujitenga na mambo yasiyo na maana.
Naibu Rais aliorodhesha baadhi ya mipango ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika kaunti ya Narok yakiwemo masoko ya Ntulele na Suswa yaliyokamilishwa kwa gharama ya shilingi milioni 55.